Mwanafunzi Yatima wa Isalalo Secondary Apatiwa Msaada wa Mahitaji ya Shule
Mwanafunzi Yatima wa Isalalo Secondary Apatiwa Msaada wa Mahitaji ya Shule
Mwanafunzi yatima anayejulikana kwa jina la Dorcas John Mnkondya, anayesoma katika Shule ya Sekondari Isalalo, amepatiwa msaada wa mahitaji muhimu ya shule baada ya kubainika kuwa alikuwa anakosa mahitaji hayo muhimu kwa ajili ya masomo yake.
Dorcas alibainishwa na Kamati ya MTAKUWA ya Kata ya Isalalo, kamati inayojishughulisha na kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na wanawake katika jamii. Baada ya kubaini changamoto aliyoipata ya wazazi wake wote kufariki na baaday alianza kulelewa na bibi ambaye pia amefariki hivyo hakupata msaada wowote, kamati hiyo ilichukua hatua ya kumtafutia msaada ili aweze kuendelea na masomo yake bila vikwazo.
Kupitia juhudi za wadau mbalimbali wa maendeleo, mwanafunzi huyo amepatiwa shati, sweta, viatu vya shule, turaki (soksi) pamoja na begi la madaftari ili kumwezesha kusoma katika mazingira bora zaidi.
Kwa sasa, Dorcas anaishi chini ya malezi ya Mtendaji wa Kijiji cha Isalalo, Huruma Fured Njowela, ambaye anamsaidia kuhakikisha anapata ulinzi na malezi bora wakati akiendelea na masomo yake.
Msaada huo umetolewa na Shirika la Elisha Fashion and Design Youth Foundation, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo wanaojitolea kusaidia watoto wenye uhitaji katika jamii.
Hatua hii inaonyesha umuhimu wa mshikamano wa jamii katika kuhakikisha watoto wote wanapata haki yao ya msingi ya elimu na ulinzi. Wadau wanaendelea kuhamasishwa kushirikiana kusaidia watoto walio katika mazingira magumu ili waweze kufikia ndoto zao za maisha.
Imetolewa na:
Elisha Fashion and Design Youth Foundation