EFAD Yawafikia Watoto wa Shule ya Msingi Mtumbo kwa Msaada wa Chakula
EFAD Yawafikia Watoto wa Shule ya Msingi Mtumbo kwa Msaada wa Chakula
Mkurugenzi wa EFAD Elisha Shombe akikabidhi chakula kwa Afisa Maendeleo Tumpale Mndekesye wakati wa utoaji msaada wa chakula kwa wototo wanaoishi katika mazigira magumu kwa niaba ya taasisi na wadau.
Mbozi, Songwe – Shirika lisilo la kiserikali la Elisha Youth Support Foundation (EFAD) limeendelea kuonesha moyo wa huruma kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwa kukabidhi msaada wa kilo 420 za mahindi katika Shule ya Msingi Mtumbo, wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe.
Msaada huu umelenga kupunguza changamoto ya upatikanaji wa chakula shuleni, jambo ambalo limekuwa likichangia utoro na kudhoofisha utulivu wa wanafunzi darasani. Kupitia hatua hii, EFAD imeonesha dhamira yake ya kusaidia vijana na watoto wanaokabiliwa na changamoto za kijamii na kiuchumi.
Katika mwendelezo wa jitihada zake, shirika limekuwa mstari wa mbele katika kutoa misaada mbalimbali, ikiwemo kuwapatia sare za shule watoto zaidi ya 100 katika shule za msingi. Hatua hii ni sehemu ya malengo ya taasisi hiyo ya kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kuendelea na masomo bila kikwazo cha njaa au ukosefu wa mahitaji ya msingi.
Aidha, viongozi na wajumbe wa shirika wameikumbusha jamii kuwa na mshikamano wa kijamii kwa kuonyesha utu wa kiafrika, kushirikiana katika malezi ya watoto na kuhakikisha kuwa vijana wanathaminiwa kama msingi wa taifa la kesho. Wamewataka wazazi na walezi wa wilaya ya Mbozi, licha ya kuwa wazalishaji wakubwa wa mahindi, kuongeza jitihada za kushirikiana na wadau katika kutoa chakula na kuimarisha elimu ya watoto wao.
BONYEZA KUTAZAMA TUKIO LA UTOAJI CHAKULA HAPA