MKONO WA UPENDO KWA WATOTO WA TUPENDANE
MKONO WA UPENDO KWA WATOTO WA TUPENDANE
Elisha Fashion and Design Youth Support Foundation imeendelea kuthibitisha kuwa ubunifu unaweza kuwa daraja la matumaini pale unapogusa maisha ya wenye uhitaji. Kupitia kampeni yao ya kusaidia watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, taasisi hiyo imefika mpaka Dodoma, mtaa wa Kikuyu Mission, katika kituo cha TUPENDANE kinachowalea watoto wenye uhitaji maalum.
Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wenye moyo wa huruma, tumefanikiwa kukusanya kilo 120 za unga, ambazo zilitumwa na kukabidhiwa rasmi jana kwa watoto wanaolelewa kituoni hapo. Msaada huu umekuja wakati muafaka, ukilenga kuimarisha lishe na kuwapatia faraja watoto ambao maisha yao yamejaa changamoto nyingi.
Uongozi wa kituo cha TUPENDANE wamepokea mzigo huo kwa furaha na shukrani nyingi, wakisisitiza kuwa msaada huu utawasaidia kuendelea kuwahudumia watoto kwa upendo na kujenga mazingira salama kwao. Elisha Fashion and Design inaamini kuwa kila mtoto anastahili kutabasamu, kuthaminiwa na kupewa nafasi ya kufikia ndoto zake, bila kujali mazingira anayokulia.
Kupitia jitihada hizi, tunawakaribisha wadau wengine kuungana nasi katika safari ya kubadilisha maisha. Pamoja tunaweza – tuwapende, tuwajali, tuwatengenezee kesho yenye mwanga.